Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete atahudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Robert Mugabe wa
Zimbabwe kesho, Jumatano, Agosti 22, 2013 mjini Harare.
Rais
Kikwete na ujumbe wake ameondoka nchini jioni ya leo, Jumatano, Agosti
21, 2013, kwenda Harare kuhudhuria sherehe hizo zinazofuatia ushindi wa
Rais Mugabe na chama chake cha ZANU-PF katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika
nchini humo Julai 31, mwaka huu, 2013. Katika uchaguzi huo, Rais Mugabe
alipata asilimia 61 ya kura zote.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
21 Agosti, 2013
WAHUDUMU WA ZAHANATI WATUHUMIWA KUFANYA NGONO NA WAGONJWA
Watumishi wawili katika zahanati ya Mwanhala wilayani Nzega, wamekumbwa na kashfa ya kufanya mapenzi na wagonjwa hospitalini.
Kutokana
na kashfa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Bitun Msangi, ameiagiza
Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa
watumishi hao.
Agizo la mkuu huyo limetolewa hivi karibuni, baada
ya Diwani wa kata ya Utwigu, Sawaka Shita kuwalalamikia watumishi hao
mbele ya Baraza la Madiwani, kwa kukithiri kufanya mapenzi na wagonjwa
nyakati za kazi, licha ya kuonywa kwa mara kadhaa.
Diwani huyo aliliambia baraza hilo kuwa vitendo hivyo vinahatarisha maisha ya watumishi hao na ya
wananchi, hususani waliotembea nao na kutishia kuvunja ndoa za wananchi.
Alidai
kuwa taarifa hizo za malalamiko, zilishafika katika ofisi ya Mkurugenzi
Mtendaji, tayari kwa utekelezaji, lakini wananchi wa kata hiyo
walitaka kuifunga zahanati hiyo, baada ya kukithiri vitendo hivyo vya
kufanya mapenzi katika wodi zilizopo.
Aliomba baraza liwahamishe
na kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watumishi hao, ambapo majina
yao yamehifadhiwa kwa usalama wao, huku jitihada za kuwachukulia hatua
zikifanyika.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Patric Mbozu
alisema suala hilo ni la hatari na linapaswa kufuatiliwa kwa umakini
ili lipatiwe ufumbuzi na wananchi waendelee kupatiwa huduma za tiba.
Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri hiyo, Abraham Mdeme alikiri kupokea malalamiko
hayo na kuahidi kuwa suala hilo, litafuatiliwa mapema ikiwemo
kuwahamisha kwa kufuata taratibu zilizopo.
Mkuu wa Wilaya ya
Nzega, Msangi alisema watumishi hao, wamevunja maadili ya afya, hususani
kufanya ngono katika wodi za zahanati kwa nyakati za kazi.
Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa
makatibu wakuu kumi na mmoja na naibu makatibu wakuu 14 wapya katika
wizara mbalimbali.Miongoni mwa walioteuliwa ni Katibu Mtendaji wa Tume
ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Sifuni Mchome ambaye sasa anakuwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na aliyekuwa Mganga
Mkuu wa Serikali, Dk Deodatus Mtasiwa ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu,
Tamisemi.
P.T
Mtasiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni walisimamishwa kazi na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Februari, mwaka jana kupisha uchunguzi dhidi
yao, kutokana na kukithiri kwa migomo ya madaktari nchini, pamoja na
utendaji wao kulalamikiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema: "Mtasiwa ameteuliwa
kwa kuwa uchunguzi dhidi yake haujaonyesha kuwa ana kosa lolote, lakini
wenzake (Nyoni) na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini,
David Jairo bado wanachunguzwa.
Katika uteuzi huo, aliyekuwa Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo amehamishiwa Ikulu kusimamia
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), kuwa Naibu Mtendaji Mkuu mwenye
jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo.
Makatibu wakuu walioachwa kwa maelezo
kuwa watapangiwa kazi nyingine ni Sethi Kamuhanda (aliyekuwa Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), Kijakazi Mtengwa (Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto) na Omary Chambo (Uchukuzi), huku aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick
Rutabanzibwa akistaafu wa hiari.
Balozi Sefue alisema Rais Kikwete
ameanzisha kitengo kipya katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi),
kitakachokuwa kikishughulikia afya ambacho kitasimamiwa na Dk Mtasiwa.
Aidha, aliwataja makatibu wakuu
waliohamishwa wizara kuwa ni Florens Turuka kutoka Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu na Joyce Mapunjo kutoka
Viwanda na Biashara kwenda Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Makatibu wakuu wapya
Alisema Jumanne Sagini ambaye alikuwa
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), ameteuliwa kuwa
Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Dk Servacius Likwelile ambaye alikuwa
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara
hiyo. Dk Patrick Makungu ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Tekinolojia pia ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa
wizara hiyo.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu (Tamisemi), Alfayo Kidata ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Dk Shaaban Mwinjaka aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Uchukuzi. Uledi Mussa ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara
ya Viwanda, Biashara na Masoko.
Charles Pallangyo aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu sasa anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya
Afya. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto, Anna Maembe ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Sihaba Nkinga ambaye alikuwa Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni ameteuliwa kuwa
Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Sophia Kaduma ambaye alikuwa Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika pia ameteuliwa kuwa Katibu
Mkuu wa wizara hiyo.
Naibu makatibu wakuu wapya
Naibu makatibu wakuu wapya wizara zao
katika mabano ni Angelina Madete (Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira),
Regina Kikuli (Ofisi ya Waziri Mkuu), Zuberi Samataba (Ofisi ya Waziri
Mkuu-Tamisemi anayeshughulika na Elimu), Edwin Kiliba (Ofisi ya Waziri
Mkuu-Tamisemi), Dk Yamungu Kayandabila (Kilimo, Chakula na Ushirika),
Profesa Adolf Mkenda (Fedha-Sera), Dorothy Mwanyika (Fedha-Fedha za Nje
na Madeni), Rose Shelukindo (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Dk
Selassie Mayunga (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi), Monica
Mwamunyange (Uchukuzi).
Consolata Mgimba (Elimu na Mafunzo ya
Ufundi), Profesa Elisante ole Laizer (Habari, Utamaduni na Michezo) na
Armantius Msole (Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
Waliohamishwa
Naibu makatibu wakuu waliohamishwa ni
John Mngodo (Uchukuzi kwenda Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia),
Selestine Gesimba (Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwenda Wizara ya
Maliasili na Utalii).
Injinia Ngosi Mwihava (Ofisi ya Makamu
wa Rais kwenda Wizara ya Nishati na Madini), Maria Bilia (Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi kwenda Viwanda na Biashara na Nuru Milao
(Maliasili na Utalii kwenda Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto).
Aidha, Dk Donaldo Mbando
amethibitishwa kuwa Mganga Mkuu wa Serikali baada ya kukaimu nafasi hiyo
tangu kusimamishwa kwa Dk Mtasiwa.
WANANCHI KILOMBERO WANUFAIKA NA MRADI WA MAJI YA VISIMA
Akina mama wa Kilombero wakiandaa mlo
kwa ajili ya timu za Help for Underserved Communities (HUC) na Lifetime
Wells for Ghana Inc., wakati wa ufungaji pampu katika moja ya visima
Wilaya ya Kilombero, Morogoro, uliofanyika hivi karibuni. Zaidi kuhusu
mradi huu bofya;
www.facebook.com/pages/Help-for-Underserved-Communities-HUC-USA. (Picha
zote na Nathan Mpangala wa HUC)
P.T
Mtoto toka Kilombero, akifuatilia
ufungaji pampu katika moja ya visima 59 uliofanywa na timu za Help for
Underserved Communities (HUC) na Lifetime Wells for Ghana Inc., Wilaya
ya Kilombero, Morogoro, hivi karibuni.
Haya twende! Timu ya Help for
Underserved Communities (HUC) ikishirikiana na Lifetime Wells for Ghana
Inc., wakichimba moja ya visima 59 Wilaya ya Kilombero, Morogoro, huku
wakiangaliwa kwa shauku na watoto hivi karibuni. HUC ni asasi isiyokuwa
ya kiserikali yenye makao yake Marekani, inayochimba visima kwa
kushirikiana na jamii kusaidia upatikanaji wa maji ya kunywa safi na
salama mashuleni, vijijini na jamii kwa ujumla. Zaidi, bofya;
www.facebook.com/pages/Help-for-Underserved-Communities-HUC-USA.
Mwanasiasa wa Sweden ajeruhiwa Somalia;
Watu waliokua na silaha wamewaua watu
wawili na kumjeruhi mwanasiasa wa Sweden Ann-Margarethe Livh baada ya
kushambulia gari lake mjini Mogadishu, Somalia.
Maafisa wanasema watatu hao
walishambuliwa wakati wakirejea katika hoteli ya mwanasiasa huyo baada
ya kutoa hotuba kuhusu demokrasia katika chuo kikuu mjini humo.
P.T
Hakuna kundi lililodai kutekeleza
shambulio hilo wala sababu za kumlenga Bi Livh. Somalia inakabiliwa na
maasi ya wanamgambo wa kiisilamu wa Al Shabaab ambapo pia inakumbwa na
visa vya jinai.
Wiki jana shirika la misaada la
Medecins Sans Frontier{MSF} lilitangaza kufunga huduma zake zote nchini
Somalia kutokana na mashambulio dhidi ya wafanyikazi wake.
Somalia imekua bila serikali thabiti tangu kuondolewa madarakani kwa utawala wa Siad Barre mwaka wa 1991.
Duru za usalama zimesema Bi Livh
amepokea matibabu katika hospitali ya wanajeshi wa Muungano wa Afrika
mjini Mogadishu. Msemaji wa chama cha Ann-Mararethe Livh amesema
mwanasiasa huyo alipata majeraha ya risasi.
Kwa sasa kuna mipango ya kumsafirisha
hadi mjini Nairobi, Kenya kwa matibabu zaidi.Familia yake imesema
mwanasiasa huyo alikua shwari licha ya majeraha.
Takriban wanajeshi 18,000 wa Muungano
wa Afrika wanashika doria nchini Somalia ili kusaidia serikali mpya ya
Somalia. Utawala wa sasa ndio wa kwanza kutambuliwa na Umoja wa Mataifa,
Marekani na Shirika la Fedha duniani kwa zaidi ya miongo miwili.
Wapiganaji wa Al Shabaab wameondolewa
mjini Mogadishu lakini wanathibiti maeneo kadhaa ya Somalia. Kuna
makundi mengine ya kikoo ambayo yanathibiti maeneo mengi ya Somalia.